Sunday, July 17, 2011

Msechu: Mimi na Juliana ni sanaa tu

KATI ya washiriki wa shindano la Tusker Project Fame All Stars, linaloendelea hivi sasa jijini Nairobi ambalo limewashirikisha mastaa wa shindano hilo miaka ya nyuma kutoka nchi zote Afrika Mashariki huwezi kukosa kumtaja Peter Msechu.

Msechu ambaye amekuwa kivutio cha wengi katika jukwaani la All stars, pia ni msanii mahiri hata asimamapo pekee, na kufanya kazi zake binafsi za kimuziki tofauti na awapo katika mashindano mbalimbali aliyowahi kushiriki.

Bongo Star Search ndio shindano lililoibua kipaji cha Msechu, hata hivyo alishindwa kuibuka kidedea na kushika nafasi ya pili. Ikiwa ni ishara kwamba ana kipaji, Msechualiweza kuchaguliwa kuingia katika shindano la Tusker Project Fame msimu wa 4 na aliweza kushika namba mbili, na hivi tunavyoongea Msechu anaiwakilisha tena Tanzania katika msimu wa 5 wa All Stars.

Tulifanya mahojiano ya ana kwa ana na Msechu na katika mazungumzo aligusia suala ya Watanzania kuwa wazalendo na kujali kile ambacho Mtanzania mmoja anakifanya nje ya nchi kama moja ya kujenga Taifa lake.

Mwandishi: Tangu kuanza kwa shindano la All Stars umekuwa ukishika nafasi ya pili kila wiki unadhani Watanzania wategemee ushindi kwa Tusker mwaka huu.

Msechu: Nawaomba sana Watanzania wawe wazalendo kwa kunipigia kura kwa wingi ili Tanzania nayo mwaka huu iibuke mshindi katika mashindano haya. Nashkuru Mungu mwaka jana nilipigiwa kura nyingi lakini hazikutosha kuweza kuniweka kinara. Unaweza kumpigia kura Msechu kwa kuandika neno TUSKER unaacha nafasi kisha kwenda namba 15324 na inagharimu shilingi 50 tu.

Mwandishi: Unadhani kura ndio sababu ya wewe kushindwa mwaka jana?

Msechu: Nadhani, kwani ikiwa Watanzania wangepiga kura za kutosha bila shaka ningepeta ushindi wa kishindo kama ilivyokuwa kwa Davis. Watanzania wategemee ushindi ikiwa watapiga kura kwani ni idadi kubwa ya mashabiki ambao hawaangalii nchi wananipigia kura na nashkuru kwa hilo. Mimi ni Msechu nawakilisha Tanzania, hivyo itakuwa fahari kwa Tanzania ikiwa nitashinda.

Mwandishi: Katika mashindano ya mwaka huu na mwaka jana kuna utofauti wowote unaouona?

Msechu: Kuna tofauti kubwa sana, kwanza hii ni All Stars namna ya ushiriki ni tofauti sana na mwaka jana, kwani mwaka jana tulikuwa tukiishi katika shule maalum ya muziki huku tukipewa mafunzo, hiyo ni tofauti na mwaka huu, kwani hivi sasa tunaishi hotelini na si kama wanafunzi kama zamani bali ni mastaa ambao tunajua nini tunafanya

Mwandishi: Kuna ugumu wowote katika mashindano ya All Stars?

Msechu: Kwangu naona ni mteremko tu, kwani nina mashabiki wengi. Lakini kuna sehemu kwangu naiona ngumu hasa katika kugawana mashabiki. Tuliopo ni mastaa na kila staa ana mashabiki wake sasa ugumu unakuja ni namna gani nitaweza kuwachukua mashabiki wa Davis au Alpha hili ndio ninahangaika nalo kwa sasa.

Mwandishi: Vipi kuhusu suala la kumwimbia Juliana Kanyomozi je unamaanisha? Mwaka jana ulisema ni sanaa na mwaka huu unasemaje?

Msechu: Bado ni sanaa, na itabaki kuwa sanaa kwani kila msanii lazima awe na mbinu za kuwavuta mashabiki upande wake, hivyo mwaka jana nilipata fursa ya kukusanya mashabiki kupitia Juliana hivyo mwaka huu niliona nianze na hilo ili kuwakumbusha mashabiki lakini aluta continua! (mapambano yanaendelea)

Mwandishi: Unawaahidi nini Watanzania katika All Stars

Msechu: Ninaahidi kwamba nitafika fainali nikiwa nacheza katika namba tatu kama nilivyoanza na zaidi nategemea ushindi kwani nimejipanga sawasawa mwaka huu katika kuufikia ushindi.

Mwandishi: Ni nini ambacho unahisi umekikosa ndani ya kipaji chako?

Msechu: Shule! Shule imekuwa tatizo kwangu, mwaka jana nilipata sponsor kutoka Tusker Project Fame ya kusoma ilikuwa ni kozi ya muda mfupi, lakini kule nilikwenda kukuta mambo ya utabibu, nilishindwa kwani mpango wangu ni kusomea zaidi muziki niujue zaidi ili niweze kufikia malengo yangu kimaisha. Hivyo nahitaji ufadhili ili niweze kusoma zaidi kuhusu muziki.

Mwandishi: Umeshatoa single mbili mpaka sasa, una mpango wa kutoa albamu?

Msechu: Baada ya Hasira hasara na Unaniumiza niliyoimba na Bella Kombo wa BSS nina mpango wa kufanya kolabo na Kidumu na mwanadada Juliana Kanyomozi, lakini sina mpango wa kutoa albamu, kwani hazilipi hivyo si wakati wake kwa sasa labda hapo baadaye sana.

No comments:

Post a Comment