Saturday, July 16, 2011

P-UNIT ..wanamzimia Dogo Janja!

Na Henry Mdimu
WAKATI mwingine kuvuka boda si jambo ajabu , hasa katika suala zima la kuleta burudani kwa wasomaji wetu.
Kwa mantiki hiyo, wiki hii tuliamua kukutana na wakare kutoka Codes za 254, yani Kenya. Jamaa watatu ambao wanajiita P- Unit kwa pamoja, walifika nchini kwa ajili ya shoo moja nzuri ya ufukweni. Shoo hiyo iliyofanyika siku ya Jumamosi.

‘Si lazima’ ndio ngoma iliyowatambulisha kwenye medani ya muziki, lakini ukiachana na hiyo, Hivi sasa wamepanda juu katika chati za muziki Afrika Mashariki. Baadhi ya kazi zao zinazotamba kwa sasa ni pamoja na ‘ Kala kare’, ‘Hapa kule’ na ‘Kathaa’.

Katika kudhihirisha uzalendo jamaa hao hawakumwacha mbali mshkaji wao Nonini na hivyo kumshirikisha.
Rekodi tuliyonayo mpaka sasa ni kwamba, P-Unit wanashikilia jumla ya tunzo nane, huku kundi likiwa na miaka mitano kwenye ‘game’. Kwa upande wa sokoni jamaa wana albam moja tu, ambayo inafanya vizuri sana inayokwenda kwa jina la ‘Wagenge hao’ iliyotoka mwaka jana.

Unataka kujua tunzo zao?
Mwaka 2007 kupitia tunzo za Chaguo la teeniez ngoma yao ya ‘Si lazima’ ikachukua tunzo ya wimbo bora wa kushirikiana, pia ukawa wimbo bora wa mwaka, na P Unit likawa kundi bora la mwaka huo pia.

...tatu hizo!

Mwaka huo huo pia wakatunukiwa tunzo ya nne na ‘Kisima Awards’ kama kundi bora la mwaka.
Tunzo ya tano waliyoipata, ikaja tena kutoka Teeniz mwaka 2008, na Kisima tena wakawapa tunzo ya sita mwaka huo huo wa 2008 kwa kuwa kundi bora tena. Wakati huo wakiwa wameshatoa ngoma moja kali iliyokwenda kwa jilna la ‘Una’ wakiwa wamemshirikisha DNA ngoma ambayo pia ilichukua tunzo ya ngoma bora ya kushirikiana.

Kama hilo halitoshi jamaa wamewahi pia kutajwa mara mbili katika tunzo za MTV, mara ya kwanza ilikuwa kupitia ngoma ya ya ‘Una’, ambayo ilitajwa kuwania tunzo za MTV kama ngoma inayosikilizwa sana redioni.

Mwaka jana, yaani 2010, waliwania tunzo ya kundi bora ya muziki.
Hawa ni Gabuu, Boni na Frasha, ambao wikiendi hii walikuwa karibu na Mwandishi Wetu Henry Mdimu, na kupiga naye mahojiano katika hoteli ya Regency iliyopo jijini Dar es Salaam.

Mwandishi: Miaka mitano bila kukwaruzana na kuishi kwa furaha kama hivi ni hatua ndefu sana. Je, ni nini siri ya mafanikio?

Gabuu: Si kweli eti kwamba hatukwaruzani, tunapishana sana na tunabishana kila mara lakini tunaichukulia kama sehemu ya maisha na ndio maana mpaka leo unatuona tunaishi kama familia. Siku zote tunaamini kuwa, matatizo ya P- Unit ndio matatizo ya kundi jingine, huwezi kukimbia hapa ukaenda kwingine eti ukakuta kitu tofauti.
Frasha:...na pia tunaishi kama familia.

Mwandishi: Hivi Nonini amejitoa P-Unit?
Boni: Hakuwahi kuwa ‘member’ wa kundi ila ni mtu wetu wa nguvu, ambaye tunafanya naye kazi kwa karibu kabisa. Na ukweli ni kwamba, yeye ndiye aliyetutambulisha kwenye ‘game’, kama unakumbuka kwenye ‘Si lazima’ ‘intro’ alisema, "Introducing, ..Boni and Frasha, ..na Gabuu".

Gabuu: Pale ndio alimaliza mchezo, alitutambulisha kwenye ulimwengu wa muziki na ndio sasa twatembea kwa miguu yetu kama hivi.

Mwandishi: Katika miaka mitano ni albam moja tu, mmewahi kufanya au mnasumbuliwa na uharamia katika game kama ilivyo kwa Tanzania. Je, hilo mnaliongeleaje?
Gabuu: Hilo ni tatizo la dunia nzima. Tanzania na kenya ni sawa sawa tu, ila tunajaribu kufanya kila linalowezekana tusiibiwe. Bado hakujakuwa na soko imara na udhibiti wa nguvu bwana. Uharamia huo ndio sababu iliyofanya albam yetu kutouzwa Tanzania. Na ndio maana kila ngoma tukitoa mnaoina kama ni mpya.

Pamoja na hilo, huwa tunauza nyimbo zetu mitandaoni na tuna mkataba na Safaricom ambapo mtu unaweza kununua ngoma kupitia simu ya mkononi.

Mwandishi: Kwa Tanzania kuna msanii gani mnamzimia?
Gabuu: AY, Binamu, Chidbenz...

Frasha: weengi wengi bana Marlaw, Jaydee..
Boni: Na yule mtoto wa Manzese..Dogo Janja, tunafikiri kama tufanye naye ngoma hivi nafasi ikiwepo.
Mwandishi: Jambo jingine kubwa zuri la mwisho naona mna haraka...

Frasha: ..tuna haraka tunataka tukamange kidogo mazee...
Gabuu: Tuna ngoma mpya inakuja ni surprise, hata hutajua kama ni P Unit mpaka utakapotajiwa ndio utakubali, ni mapinduzi makubwa katika muziki tunaofanya.

Mwandishi: Kila la heri jamani.
Frasha: ..karibu Kenya!

No comments:

Post a Comment